Rais Kenyatta atoa hati ya kibali kwa Chuo Kikuu cha Presbyterian

Taasisi ya Elimu ya Juu ya Presbyterian of East Africa sasa imekuwa Chuo Kikuu kamili baada ya kupewa hati ya kibali na Rais Uhuru Kenyatta.

Akiongea wakati wa hafla ya kutoa hati hiyo rasmi kwa chuo hicho katika Ikulu ya Nairobi Jumatano, Rais alihimiza chuo kikuu hicho kipya kutoa mafunzo ambayo yataleta suluhu kwa changamoto za sasa zinazowakumba wanadamu.

“Chuo Kikuu hiki kina hadhi zote za kuwa msitari wa mbele katika eneo hili na ulimwenguni kote kutoa elimu ya juu, utafiti na maendeleo, uvumbuzi na utoaji wa suluhu kwa changamoto za sasa,” akasema Rais.

Alisema serikali inajivunia kujumuisha kanisa kama mshirika halisi wa maendeleo ya kitaifa hasa katika kuwa na maono sawa ya nchi bora zaidi na yenye ufanisi kwa wote.

“Kanisa hapa Kenya limehusika pakubwa katika maisha ya taifa hili. Mbali na kulisha nafsi na roho kupitia kueneza Injili, kanisa pia limefuata nyayo za Kristo kwa kuanzisha shule, hospitali, vituo vya kutoa chakula na mipango ya kusaidia jamii,” akaongeza Rais.

Kuhusu mpango unaoendelea ya kuzindua mtalaa mpya wa elimu, Rais alisema Wizara ya Elimu itaendelea kushirikiana kwa karibu na vyuo vikuu vyote ili kuhakikisha vinatoa wasomi wenye uadilifu kuongoza marekebisho katika sekta ya elimu.

Rais alivitaka vyuo vikuu kuanza kujiandaa kuwapokea na kuwafunza wanafunzi wanaofuzu kutoka kidato cha nne chini ya mtalaa mpya wa elimu akisema maandalizi ya vyuo vikuu hivyo ndiyo yatahakikisha mtalaa huo mpya unafaulu humu nchini.

Kiongozi wa nchi alikipongeza chuo kikuu hicho cha Presbyterian kwa kutoa mafunzo bora yanayokuza wanafunzi wanaofuzu wenye uadilifu na pia maadili mema.

One thought on “Rais Kenyatta atoa hati ya kibali kwa Chuo Kikuu cha Presbyterian

  • 3 December 2020 at 11:56 am
    Permalink

    Nami nilikua karibu na utozi wa kibali cha Presbyterian University kua chuo kuu Kamili

    Reply

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *