Rais Kenyatta ataka mazungumzo ya amani kukomesha mzozo nchini Ethiopia

Rais Uhuru Kenyatta amejiunga na viongozi wengine wa kimataifa kutaka mapigano kaskazini mwa Ethiopia yakomeshwe kupitia njia ya mazungumzo.

Kwenye ujumbe wake kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Kenyatta ametahadharisha kuhusu athari za mzozo huo kwa nchi hizi mbili, ambazo zimekuwa wasuluhishi wa mizozo katika kanda hii navielelezo vya amani na uthabiti

Rais alisema hayo baada ya kukutana na Naibu Waziri Mkuu wa Ethiopia, aliye pia Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo Demeke Mekonen katika Ikulu ya Nairobi.

Mekomen pia alimpa Rais Kenyatta ujumbe maalum kutoka kwa Waziri Mkuu wa Ethoipia Abiy Ahmed kuhusu maswala mbali mbali ikiwemo hali ya siasa na usalama Ethiopia.

Kwenye mkutano huo, Rais Kenyatta alikuwa ameandamana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni humu nchini Raychelle Omamo, Katibu wake Ababu Namwamba na Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt. Joseph Kinyua.

Viongozi kadhaa wa kimataifa wamewataka wapiganaji wa kundi la TPLF kusitisha  mapigano ambayo yanavuruga mafanikio yaliyokuwa yamepatikana na kutatiza juhudi za Ethiopia za kustawisha nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *