Rais Kenyatta aongeza kafyu hadi mwezi Machi

Rais Uhuru Kenyatta ameongeza muda wa kafyu hadi tarehe 12 mwezi Machi mwaka huu.

Hii inafuatia kumalizika kwa muda wa awali wa kafyu uliowekwa mwezi Novemba mwaka uliopita, ambao ulitarajiwa kumalizika usiku wa manane Jumapili.

Kafyu itaendelea kuzingatiwa kati ya saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri.

Agizo hilo pia linahusisha masharti mengine ya kukabiliana na msambao wa ugonjwa wa COVID-19.

Tangazo hilo limetolewa Jumapili na Waziri wa Usalama wa Kitaifa  Dkt. Fred Matiang’i wakati wa kutoa taarifa kuhusu maandalizi ya serikali na sekta ya elimu, huku wanafunzi wakitarajiwa kurejea shuleni Jumatatu.

Wakati wa utoaji taarifa katika jumba la KICC, Waziri wa Elimu Profesa George Magoha amesema serikali itatoa barakoa milioni tatu kwa wanafunzi wanaohitaji kusaidiwa wakati shule zinapofunguliwa.

Amewaomba wazazi walio na uwezo wawanunulie watoto wao angalau barakoa mbili.

Waziri hata hivyo amekiri kwamba haitakuwa rahisi kutimiza masharti ya wanafunzi kukaa umbali wa mita moja madarasani.

Amekariri kwamba shule zinapasa kutenga nafasi zaidi kwa wanafunzi chini ya mti, kwenye vyumba vya mankuli na maeneo mengine yaliyo wazi.

Profesa Magoha pia amesema serikali imetoa shilingi bilioni nne kwa mpango wa elimu bila malipo katika shule za msingi.

Amesema shule za sekondari zitapokea shilingi bilioni 14.6 ifikapo ijumaa wiki ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *