Rais Kenyatta aomboleza kifo cha Mbunge wa Juja Francis Munyua Waititu

Rais Uhuru Kenyatta amejiunga na viongozi wengine katika kutuma risala za rambirambi kwa familia jamaa na wakazi wa eneo bunge la Juja kufuatia kifo cha mbunge wao Francis Munyua Waititu.

Kwenye risala yake, Rais Kenyatta amemtaja Waititu ambaye alifahamika kama  ‘Wakapee’, kama kiongozi mkakamavu, mwaminifu na mwenye kujitokea.

Mbunge huyo alifariki jana jioni katika Hospitali ya MP Shah, Nairobi baada ya kuugua maradhi ya saratani.

Wakapee alichaguliwa kuwa mbunge wa Juja mwaka wa 2013 na baadaye kuhifadhi kiti chake mwaka wa 2017.

Amekuwa akiugua saratani ya ubongo kwa muda mrefu na aliwahi kusafiri hadi India kwa ajili ya matibabu.

Mbunge huyo alikuwa ameahidi mradi wa ujenzi wa kituo cha kukabiliana na saratani katika Kaunti ya Kiambu.

Mbunge wa Kiambaa, Paul Koinange kwenye risala yake amemtaja mbunge huyo kama kiongozi aliyewapenda watu ambaye alitangamana vyema na wabunge na pia wananchi.

Koinange ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usalama wa taifa bungeni, amedokeza kuwa Waititu alichangia vyema mijadala na kutangamana vyema na wabunge wenzake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *