Rais Kenyatta amuomboleza Mbunge wa Matungu Justus Murunga

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa familia, jamaa, marafiki na wakazi wa Eneo-Bunge la Matungulu kufuatia kifo cha Mbunge wa eneo hilo Justus Murunga Makokha.

Kwenye risala yake, Rais amemtaja mwendazake kama mtu mkakamavu aliyejitolea kuwahudumia na kuinua maisha ya wakazi wa eneo lake.

“Katika wakati huu wa maombolezo, natuma rambirambi zangu kwa familia ya Murunga, jamaa na wakazi wa Eneo-Bunge la Matungulu. Mawazo na maombi yangu ni pamoja nanyi,” amesema Rais.

Mbunge huyo wa awamu ya kwanza anayeegemea upande wa upinzani aliripotiwa kufariki Jumamosi jioni alipokuwa akipelekwa hospitalini huko Mumias baada ya kuzirai nyumbani kwake.

Kilichosababisha kifo cha mbunge huyo bado hakijabainishwa, huku kukiwa na madai kwamba huenda kimetokana na ugonjwa wa COVID-19.

Rais Kenyatta amewatakiwa waombolezaji faraja wakati wanapokabiliana na maombolezo kufuatia kifo cha kiongozi wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *