Rais Kenyatta amtembelea mwenzake wa Italia, wajadili biashara na vita dhidi ya COVID-19

Rais Uhuru Kenyatta alimtembelea mwenzake wa Italia Sergio Mattarrella wakati huu ambapo anaendelea na ziara rasmi katika makao makuu ya Vatica.

Kwenye ziara hiyo, Rais Kenyatta amekusudia kuboresha uhusiano wa muda mrefu kati ya Kenya na Italia kama mshirika muhimu wa maendeleo.

Viongozi hao wawili wamejadili kuhusu njia za kuimarisha uhusiano wa kibiashara, uwekezaji na utalii.

Aidha, wameshauriana kuhusu namna ambavyo Kenya na Italia zinaweza kubadilishana mawazo kuhusu njia bora za kupambana na msambao wa COVID-19.

Italia ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi kote duniani na ugonjwa wa COVID-19 baada ya kuandikisha vifo vya zaidi ya watu elfu 40.

Jinsi ilivyo hapa nchini Kenya, Italia inapambana na wimbi la pili la ugonjwa wa COVID-19.

Italia ni miongoni mwa nchi zinazotegemewa zaidi Kenya kwa biashara ya utalii na uwekezaji.

Mnamo mwaka wa 2019, Kenya iliuza bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 kwa taifa hilo la Bara Ulaya, kiwango ambacho kilikuwa cha chini kwa kulinganisha na mwaka wa 2018 ambapo pato hilo lilikuwa shilingi bilioni 3.9.

Kenya inatafuta kuboresha zaidi uhusiano wake na Italia  kukiwa na lengo la kuvutia wawekezaji zaidi wa taifa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *