Rais Kenyatta ampongeza Rais wa Ghana Akufo-Addo kwa kuchaguliwa tena

Rais Uhuru Kenyatta amempongeza mwenzake wa Ghana Nana Akufo-Addo kwa kuchaguliwa kwa kipindi cha pili nchini humo.

Rais Kenyatta amesema ushindi wa Akufo-Addo kwenye uchaguzi huo uliokuwa na upinzani mkali ni dhihirisho la imani waliyonayo raia wa Ghana kwa maono ya kiongozi huyo.

“Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Kenya na kwa niaba yangu mwenyewe, natoa pongezi zangu za dhati kwa kuchaguliwa kwako tena kama rais wa Ghana,” akasema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta pia amekariri kwamba chini ya uongozi wa Akufo-Addo, Ghana itazidi kushuhudia maendeleo zaidi yale yaliyoonekana wakati alipokuwa akihudumu kwa kipindi cha kwanza, kwa ajili ya manufaa ya raia wa Ghana na pia Bara zima la Afrika.

Kiongozi wa taifa pia ameelezea matumaini yake ya kushirikiana na huyo wa Ghana ili kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kimaendeleo kati ya nchi hizo mbili.

Amemtakia afya njema anapoanza kuhudumu katika awamu ya pili kama rais wa Ghana.

Rais Akufo-Addo alitangazwa mshindi baada ya kupata asilimia 51.6 ya kura zilizopigwa na kumpiku mpinzani wake wa karibu John Mahama ambaye alipata asilimia 47.4 ya kura hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *