Rais Kenyatta ampongeza Rais Mteule wa Marekani Joe Biden

Rais Uhuru Kenyatta ,amempelekea risala za pongezi Rais Mteule wa Marekani Joseph Robinette Biden kufuatia kuchaguliwa kwake katika uchaguzi wa hivi punde nchini Marekani.

Katika risala yake Rais Kenyatta alitaja ushindi huo katika uchaguzi ulioshuhudia kinyang’anyiro kigumu, kuwa dhihirisho la imani ya watu wa Marekani katika uongozi wa  makamu huyo wa rais wa zamani.

”Wamarekani wameongea kwa sauti kubwa kupitia kwa kura zao na kumchagua kiongozi mwenye  tajriba,mwenye sifa nyingi na pia kiongozi wa muda mrefu kuwa kiongozi wa Ikulu.

Kwa niaba ya wananchi na serikali ya Kenya,Nampongeza Rais mteule Joe Biden na makamu Rais  Mteule  Kamala Harris kwa ushindi wao mkubwa na kuwatakia kila la heri  wanapojiandaa kuongoza Marekani kwa ufanisi wa siku za usoni” akasema Rais

Rais Kenyatta amemtaja Rais Mteule kuwa rafiki wa Kenya ambaye ziara yake ya mwisho  humu nchini  akiwa makamu wa rais wa Barack Obama iliimarisha ushirikiano baina ya  Kenya na Marekani.

Kiongozi wa Taifa pia amempongeza makamu wa Rais Mteule  Kamala Harris kwa kuandikisha historia kuwa mwanamke wa kwanza ,kuwa makamu wa Rais katika  historia ya siasa za Marekani.

Wakati uo huo Rais Kenyatta amemshukuru Rais anayeondoka Donald Trump na  uongozi wake kwa kuwa na uhisiano mwema na wa  karibu na  Kenya na kumtakia mema anapoiaga Ikulu ya Marekani White House.

Rais Mteule Joe Biden akiwa na Raila Odinga katika ziara yake nchini Kenya akiwa makamu wa Rais Obama

Viongozi wengine wa Kenya waliompongeza Rais Mteule Joseph Biden ni Kiongozi wa ODM Raila Odinga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Joe Biden akiwa na Rais Mstaafu Mwai Kibaki ,Raila Odinga na Kalonzo Musyoka alipozuru Kenya

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *