Categories
Habari

Rais Kenyatta ampongeza Museveni kwa kuhifadhi kiti cha urais nchini Uganda

Rais Uhuru Kenyatta amempongeza Yoweri Museveni kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Uganda.

Siku ya Jumamosi, Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi huo mkuu kwa kujizolea zaidi ya asilimia 58 ya jumla ya kura za urai.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Museveni alimshinda mpinzani wake mkuu, Bobi Wine, aliyepata asilimia 34 ya kura hizo zilizopigwa mnamo siku ya Alhamisi.

Kupitia ukurasa wa Facebook wa Ikulu ya Kenya, Rais Kenyatta amesema kuchaguliwa tena kwa Museveni ni ushuhuda tosha wa imani waliyonayo wananchi wa Uganda kwa uongozi wake.

Kwenye ujumbe wake wa heri, Rais Kenyatta pia ameahidi kuendelea kushirikiana na Museveni ili kuimarisha zaidi uhusiano kati ya Kenya na Uganda kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Kiongozi wa taifa pia ameusifu uongozi wa Museveni kwa kuimarisha nchi hiyo na vile vile kuandikisha maendeleo bora ya kiuchumi nchni humo.

Museveni, mwenye umri wa miaka 76, amekuwa uongozini tangu mwaka wa 1986 na ushindi wake sasa unamaanisha kwamba ataiongoza Uganda kwa muda usiopungua miaka 40 kama rais.

Hata hivyo, upande wa upinzani tayari umepinga matokeo hayo, huku Bobi Wine akiahidi kutoa ushahidi wa kuonyesha kwamba kulikuwa na udanganyifu mwingi kwenye shughuli ya kuhesabu na kujumlisha kura hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *