Rais Kenyatta akutana na Waziri kutoka Japan katika Ikulu ya Nairobi

Rais Uhuru Kenyatta amekutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Japan anayezuru humu nchini, Toshimitsu Motegi, katika Ikulu ya Nairobi.

Wakati wa mkutano huo, Motegi, ambaye yuko kwenye ziara ya siku mbili humu nchini, ameeleza kuendelea kujitolea kwa Japan kuunga mkono mipango ya maendeleo humu nchini, hasa miradi ya muundo msingi.

Motegi ametaja mradi unaoendelea wa kupanua Bandari ya Mombasa na ustawishaji eneo maalum la kiuchumi la Dongo Kundu kuwa baadhi ya miradi ambayo serikali yake inamakinika kuhakikisha imekamilishwa.

Waziri huyo wa Japan pia amemuarifu Rais Kenyatta kuhusu kongamano la kibiashara kati ya Japan na Kenya ambalo litaandaliwa baadaye mwaka huu nchini Japan na akawasilisha mwaliko wa Waziri Mkuu Yoshide Suga kwake.

Kwa upande wake Rais Kenyatta ameeleza kutambua hatua ya Japan kuendelea kuunga mkono mipango ya maendeleo humu nchini, akisema nchi hii itaendelea kuimarisha uhusiano wake wa kihistoria na taifa hilo la Bara Asia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *