Rais Kenyatta akagua miradi mbali mbali ya maendeleo

Rais Uhuru Kenyatta amekagua miradi kadhaa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Kitaifa.

Kiongozi wa taifa amezuru Bandari ya Kisumu ambapo wanajeshi wa humu nchini wanajenga ua jipya la kuegeshea meli kama sehemu ya ukarabati na upanuzi wa usafiri wa majini.

Baadaye Rais amekagua mradi wa ujenzi wa Jumba la kibiahsara la Uhuru, linalojumuisha soko la kisasa katika eneo la Jua Kali huko Kisumu, unaoendelea katika ardhi ya ekari 23 zilizotolewa na Shirika la Reli nchini.

Akiandamana na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Robert Kibochi, Rais Kenyatta pia ametembelea mradi wa ujenzi wa uga wa Jomo Kenyatta katika eneo la Mamboleo utakaogarimu shilingi milioni 415.

Katika uga huo ambao ukamilifu wake umefikia asilimia 65, Gavana wa Kaunti ya Kisumu Profesa Anyang Nyong’o pamoja na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa pia walijumuika na msafara huo wa ukaguzi.

Rais Kenyatta ameridhishwa na hatua za ujenzi huo na akawasihi wajenzi kuhakikisha kwamba uwanja huo wa michezo unakamilika kufikia mwezi Aprili mwaka huu.

Kwenye safari yake ya kurejea Nairobi, kiongozi wa taifa pia amekagua ukarabati wa reli ya Nairobi kuelekea Magharibi mwa Kenya.

Aidha, amepitia katika kituo cha kuhifadhia makasha cha Naivasha ambapo Shirika la Reli linajenga kilomita 24 za reli inayounganisha reli ya kisasa (SGR) na ile inayokarabatiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *