Rais Kenyatta ajiunga na familia ya Mkurugenzi Mkuu wa NYS Matilda Sakwa katika maombolezo

Rais Uhuru Kenyatta ametuma risala za rambirambi kwa familia ya Florence Oyiela Sakwa aliyeaga dunia jana alipokuwa akitibiwa katika hospitali moja Jijini Nairobi.

Sakwa, ambaye ni mwalimu mstaafu, alikuwa mamake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), Matilda Pamela Sakwa.

Kwenye risala yake ya faraja, Rais amemwomboleza Sakwa kuwa mwalimu mahiri aliyechangia pakubwa katika ukuaji wa sekta ya elimu nchini.

“Mwalimu Florence alikuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya elimu kwa sababu alifunza watu wengi sana wanaotajika. Pia alihakikisha kwamba watoto wake wote wanapata viwango vya juu zaidi vya elimu,” akasema Rais Kenyatta.

Sakwa, ambaye alikuwa mwalimu wa somo la Kiingereza, alifunza katika shule kadhaa miongoni mwazo ile ya wasichana ya Lwak, ya Kiufundi ya Kisumu, za Sekondari za Mutuini, Dagoretti na Ofafa Jericho kabla ya kustaafu.

Rais amesema kuwa Sakwa atakoswa na Wakenya wengi hasa wasichana na wanawake aliowapa ushauri nasaha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *