Rais Kenyatta ahimiza vikosi vya KDF kuwa tayari kukabiliana na vitisho vya kiusalama

Rais Uhuru Kenyatta amehimiza vikosi vya ulinzi vya Kenya KDF kuwekeza Zaidi katika mafunzo ili kuboresha ukabilianaji na vitisho vya kiusalama.

Rais aliyasema hayo Alhamisi katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Lanet kaunti ya Nakuru wakati wa gwaridi ya kufuzu.

“Vikosi vyetu vya ulinzi vinapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto za aina mbali mbali, kudhibiti kikamilifu changamoto za kiusalama za karne ya 21 na mafunzo ya kijeshi yawiainishwe na changamoto zinanochipuza,” alisema rais.

Kiongozi wa taifa aliwahimiza maafisa hao waliofuzu kuzingatia kiapo chao cha kulinda taifa hili kutokana na aina yoyote ya uvamizi.

Rais alitoa wito kwa maafisa waliofuzu kuzingatia kikamiifu mafunzo waliopokea na  kukumbuka kila mara wajibu wao wa kutumikia taifa hili kwa nidhamu ya hali ya juu.

Chuo cha mafunzo ya kijeshi kimekuwa kikitoa mafunzo kwa maafisa wa cadet katika kanda ya Afrika Mashariki na pia katika mataifa mengine barani Afrika kama vile Botswana, Burundi, Malawi na Swaziland kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa mataifa ya Afrika mashariki.

“Nina hakika kwamba maafisa waliofuzu kutoka mataifa ya Rwanda, Tanzania na Uganda, watarejea katika nchi zao wakiwa na mafunzo ya hali ya juu kutoka kwa tasisi iliyobobea kwa utoaji mafunzo ya kijeshi barani Afrika,” alisema rais.

Rais aliwatuza maafisa waliofanya vyema katika nyanja mbalimbali wakiongozwa na Brian Mathinji Ngure aliyekuwa bora katika uogozi akifuatiwa na Diamu Dida aliyekuwa wa pili.

Gwaride hiyo ya kufuzu pia ilihudhuriwa na gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui, waziri wa ulinzi Monica Juma na mkuu wa vikosi vya KDF Jenerali Robert Kibochi.

Wengine ni pamoja na inspekta jenerali wa polisi Hilary Mutyambai na kamanda wa chuo cha mafunzo ya kijeshi Meja jenerali  Peter Njiru miongoni mwa wengine.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *