Rais Kenyatta ahimiza ushirikiano miongoni mwa viongozi, Wakenya

Rais Uhuru Kenyatta amehimiza kuwepo kwa umoja miongoni mwa viongozi na Wakenya kwa jumla ili kuafikia ajenda za maendeleo kote nchini.

Aidha, Rais amewataka viongozi wa makanisa kwa jumla kuendelea kuombea amani, umoja na maendeleo nchini.

“Nawaomba muwe na moyo wa kupendana na kushirikiana kwa sababu haya mapenzi na umoja ndio utatusaidia kuhakikisha tumejenga taifa lenye amani, nafasi za kazi na maendeleo,” amesema Rais.

Akizungumza wakati alipohudhuria ibada ya misa katika Kanisa Katoliki la Arch Angel Michael, huko Chaka Kaunti ya Nyeri, Rais Kenyatta amewakumbusha Wakenya kwamba taifa linalomcha mwenyezi mungu hufanikiwa.

Rais vile vile ameahidi msaada wake ili kukamilisha ujenzi unaoendelea wa kanisa hilo.

Baadaye Rais amezuru sehemu ambapo ujenzi wa Soko unaendelea Mjini Chaka, soko linalonuia kuwa moja kati ya masoko makubwa Zaidi humu nchini.

Amesema soko hilo litakapokamilika litatoa nafasi za biashara kwa wakazi wa sehemu hiyo pamoja na kukuza soko la mazao yao.

Rais alikuwa ameandamana na viongozi mbali mbali kutoka eneo hilo, wakiwemo Gavana wa Kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, yule wa Uchukuzi James Macharia na Mbunge wa eneo hilo Kanini Kega.

Baadaye leo alasiri Rais anatarajiwa kukutana na makundi ya vijana katika Ikulu ndogo ya Sagana.

Ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi katika eneo la Mlima Kenya ambako anashauriana na viongozi, kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *