Raila, Gavana Kingi wafokeana hadharani kuhusu chama cha Pwani

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amehitilafiana vikali na Gavana wa Kaunti ya Kilifi Amason Kingi kuhusu swala la kuundwa kwa chama cha eneo la Pwani.

Wawili hao wametupiana lawama za kisiasa jukwaani kwenye mkutano wa hadhara wa kupigia debe mswada wa BBI katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Ganze, Eneo Bunge la Ganze Kaunti ya Kilifi.

Sarakasi hiyo imeanza pale Gavana Kingi, ambaye ndiye Mwenyekiti wa ODM Tawi la Kilifi, alipomkosoa Raila kuhusu kauli yake kwamba wito wa viongozi wa Pwani kuunda chama cha kisiasa ni wa kikabila na unaotishia umoja wa kitaifa.

Kingi alikuwa anajibu matamshi ya Raila aliyoyatoa Jumanne katika Kaunti ya Taita Taveta alipoanzia ziara yake ya eneo la Pwani ya kupigia debe BBI, ambapo alisema mpango wa kuunda chama cha Pwani ni kinyume cha katiba na kuwashauri Wapwani kusalia kwenye vyama vya kitaifa.

Kutokana na matamshi hayo, Kingi amemkosoa Raila peupe na kumshtumu kwa kile alichokitaja kuwa kuwakandamiza Wapwani kila wanapojaribu kuunda mrengo wa kisiasa.

Kingi amefafanua kwamba viongozi wa Pwani hawana nia ya kusajili chama kipya bali ni muungano wa vyama kadhaa vya eneo hilo vinavyotaka kuja pamoja ili kuunda mrengo wa kisiasa wenye asili ya kiPwani.

“Hakuna chama kinaundwa hapa. Ni vyama ambavypo viko, vimetambulika kisheria kwamba ni vyama vya kitaifa vinakuja pamoja kuimarisha ngome yetu ili mwaka wa 2022 tusifungwe mabao kama siku zingine,”akaongeza gavana huyo.

Ilipofika zamu ya Raila kuhutubia, amemshtumu Kingi na kusema kuwa analeta mjadala huo kwa sababu yuko karibu kuondoka afisini. Amemkumbusha jinsi alivyomshika mkono alipokuwa bado mchanga kisiasa na hata kumpa nafasi za kuongoza wizara mbali mbali lakini sasa anazungumzia swala la kujitenga naye.

Mwaka wa 2007 nilimshika mkono mpaka nikamuweka kwa Wizara ya Afrika Mashariki, baadaye nikamleta kwenye Uchumi wa Samawati. Wakati ugatuzi ulipokuja nikamwambia asimame ugavana Kilifi nikamuunga mkono. Sasa wakati umewadia kisheria amemaliza kuwa gavana, anataka kutoroka,” amesema Raila.

Mkutano huo ni mmoja kati ya kadhaa inayohudhuriwa na Waziri Mkuu huyo wa zamani kwenye ziara yake ya eneo la Pwani ya kutafuta uungwaji mkono wa mpango wa BBI, huku kura ya maamuzi ikinukia.

Ni mkutano uliohudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Gavana Kingi, Naibu wake Gideon Saburi, Mbunge wa eneo hilo Teddy Mwambire, wabunge wengine na wawakilishi wadi mbali mbali.

Raila pia amezindua rasmi madarasa manane katika Shule ya Msingi ya Tsangalaweni ambao ni mradi wa Hazina ya Maendeleo ya eneo bunge hilo (NG-CDF) ikiwa ni moja kati ya juhudi za Mwambire za kuboresha viwango vya elimu vya eneo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *