Raila awasuta wanaopinga Huduma Namba, BBI

Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga amepuzilia mbali madai ya baadhi ya Wabunge wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto kuwa awamu ya pili ya usajili wa Huduma Namba ni njama ya kuiba kura mwaka wa 2022.

Amesema wale wanaotoa madai hayo ni viongozi wa serikalini ambao kwa kusema hivyo, huenda wanathibitisha yale waliyokuwa wakiyafanya.

Raila amesema wanasiasa hao ndio walikuwa wakimchekelea alipokuwa akizungumzia swala la wizi wa kura katika chaguzi kuu za miaka ya 2013 na 2017, kwa hivyo ni wakati wao sasa kuhisi alichokuwa akihisi yeye wakati huo.

Aidha, amewataka Wakenya kuwa tayari kwa ripoti ya BBI akisema wale walio kinyume na mpango huo wa maridhiano ya taifa na marekebisho ya katiba watashindwa.

“Wale waliozoea kupinga mabadiliko, wenye tabia ya uovu na kukwepa adhabu, wanaodumu katika ufisadi na kueneza uongo tayari wamejitokeza kupinga ripoti hiyo. Lazima tuwasimamishe katika mpango wao wa kutaka kuirudisha nchi hii nyuma,” akasema.

Akizungumza hayo wakati wa mkutano wa kamati kuu ya kitaifa ya chama cha ODM katika Kaunti ya Machakos, Raila pia amewakemea viongozi wanaotumia mali walizopata kwa njia ya ufisadi kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Amesema viongozi hao wanapaswa kudhihirisha viwango vya juu vya uadilifu kwa kuwa katika msitari wa mbele kupigana na ufisadi.

“Katika muda wa miezi michache ijayo, tutakabiliana na walionufaika na ufisadi wanaopinga ajenda yetu ya mageuzi ya kijamii na kiuchumi, kubuni nafasi za ajira na usawa katika ugavi wa rasilimali. Lazima tuwashinde.”

Ameonya dhidi ya watu kama hao ambao wanataka kuzuia taifa hili kusonga mbele waliokuwa kinyume na katiba mpya mwaka wa 2010, wakawa kinyume na maridhiano kati yake na Rais Uhuru Kenyatta, huku akielezea matumaini kuwa watashindwa kama walivyoshindwa awali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *