Raila apigia debe ripoti ya BBI Githurai

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amepeleka kampeni za kupigia debe mpango wa maridhiano wa BBI katika eneo la Githurai, Kaunti ya Nairobi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani amewataka vijana na kina mama kuunga mkono ripoti hiyo.

Raila amesema ripoti ya BBI ina manufaa makubwa kwa Wakenya endapo itaidhinishwa kwani itafanikisha kubuniwa kwa ajira na upanuzi wa biashara.

Aidha, amesema sera za BBI zitasaidia kuinua maisha ya vijana na kina mama humu nchini, kinyume cha matamshi yanayotolewa na wapinzani wa mchakato huo.

Siku ya Jumanne, ripoti ya BBI ilipata mwangaza baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuidhinisha saini za kutosha za kuiwezesha ripoti hiyo kujadiliwa bungeni.

Raila pia amesema ziara yake huko Githurai ilichochewa na suala la unyakuzi wa ardhi ambalo liliibuliwa na viongozi wa eneo hilo waliokutana naye na kuahidi kuwasilisha malalamishi hayo kwa Rais Uhuru Kenyatta ili yashughulikiwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *