Raia watatu wa kigeni wanaswa na pesa bandia Ruiru

Raia watatu wa kigeni wametiwa nguvuni wakiwa na noti bandia za takribani shilingi milioni-362, na pia madini bandia ya dhahabu katika eneo la Ruiru, kaunti ya Kiambu.

Maafisa wa upelelezi kutoka ofisi za DCI za Ruiru walivamia makaazi ya mmoja wa washukiwa katika eneo la BTL viungani mwa mji wa Ruiru jana jioni, ambako waliwanasa watatu hao.

Walionaswa ni Paulin Francis Proper mwenye umri wa miaka 44, Njikam Omar mwenye umri wa miaka 37, Job Kentong mwenye umri wa miaka 31 ambao wote raia wa Cameroon.

Maafisa wa upelelezi walipata pesa hizo zikiwa zimehifadhiwa katika masanduku ya vyuma na pia mikoba, zikiwa katika sarafu za kigeni zikiwemo dolla za Marekani, Pauni za Uingereza na pia shilingi za Kenya.

Vifaa mbali mbali pia vilinaswa, ukiwemo mtambo wa kuchapisha dolla ambao yaaminika ndio unaotumiwa kuchapisha pesa bandia.

Afisa mkuu wa DCI katika kaunti ndogo ya Ruiru Cyrus Ombati, aliwaambia wana-habari kwamba maafisa wake pia walipata kilo 250 za mawe ya dhahabu na pia miti 70 ya dhahabu.

Ombati alisema maafisa hao walikuwa wamepashwa habari kuhusu wageni waliokuwa wakijihusha na uchapishaji wa pesa bandia katika eneo la Ruiru.

Washukiwa hao wamewekwa korokoroni ili kuwasaidia polisi katika uchunguzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *