Polisi wanachunguza mauaji ya kikatili ya mwanahabari wa shirika la KBC

Maafisa wa polisi wanachunguza kisa ambapo mfanyikazi mmoja wa shirika la utangazaji nchini KBC, aliuawa kwa kupigwa risasi na majambazi Jumatano usiku.

Betty Barasa ambaye alikuwa mhariri mkuu wa video katika shirika hilo la utangazaji, alipigwa risasi ndani ya nyumba yao muda mfupi baada ya kurejea kutoka kazini.

Majambazi hao ambao inasemekana walikuwa watatu, walimfumania Betty katika lango kuu na kumshurutisha awapeleke ndani nyumba ambapo walishika mateka familia nzima.

Inadaiwa kuwa Majambazi hao waliitisha pesa kutoka kwa familia hiyo na wakati matakwa yao hayakutimizwa, walianza kuwatesa waathiriwa hao.

Huku jambazi mmoja akiachwa sebuleni na jamaa wengine wa familia hiyo, Majambazi wengine wawili waliandamana na Betty katika chumba chake cha kulala wakitafuta vitu vingine vya dhamani

Haikubainika mara moja kilichotokea katika chumba hicho cha kulala,lakini jamaa wengine wa familia hiyo walisema walisikia milio ya risasi kabla ya Majambazi hao wawili kuondoka na kuacha mwili wa Betty sakafuni ukiwa umeloa damu.

Majambazi hao kisha walichukua tarakilishi na simu moja ya rununu kabla ya kutoroka.

Tukio hilo la Jumatano jioni limeacha familia ya Betty na huzuni kubwa hasaa baada ya kushuhudia tukio lote.

Majasusi sasa wanajitahidi kukusanya  ushahidi ili kupata chanzo hasaa cha mauaji hayo ya kikatili ya mwanahabari huyo.

Waliomjua wamemwomboleza kama mwanahabari mwenye bidii na aliyejitolea huku kumbukumbu zake zikisalia katika mioyo yao dawamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *