Polisi nchini Tanzania wakanusha madai waliwaua vijana watatu kisiwani Pemba

Mkuu wa polisi nchini Tanzania, Simon Sirro, amekanusha habari kwamba maafisa wa polisi waliwauwa kwa kuwapiga risasi watu watatu Jumatatu  usiku katika mojawapo ya visiwa vya Zanzibar.

Kisiwa hicho kinatarajiwa kuandaa uchaguzi Jumatano ingawaje upigaji kura wa mapema ulianza Jumanne kwa maafisa wa uchaguzi na polisi.

Hapo awali upinzani  ulidai kwamba watu watatu waliuawa katika kijiji cha Kangagani, kaskazini mwa kisiwa cha Pemba na wengine kadhaa kujeruhiwa huku polisi wakitumia risasi kutawanya umati.

Lakini Siro aliwaambia wanahabari kwamba ni vijana 42 pekee waliokamatwa kuhusiana na ghasia huko Pemba.

Mvutano ulizuka kuhusu upigaji kura mara mbili siku ya Oktoba 27 kwa vyombo vya ulinzi na usalama na maafisa wa tume ya uchaguzi, na Oktoba 28 kwa wapiga kura wote.

Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar cha ACT-Wazalendo kilitilia shaka zoezi la upigaji kura wa mapema kikidai huenda udanganyifu ukakumba shughuli hiyo.

Muwaniaji urais kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad alitiwa nguvuni akijaribu kushiriki upigaji kura wa mapema ikizingatiwa kuwa yeye si afisa wa usalama au wa tume ya uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *