Poleni basi, Cardi B

Janga la virusi vya Corona linaendelea kuuponda ulimwengu mzima huku nchi kama vile Marekani zikiwa zimeathirika zaidi kulingana na idadi ya maambukizi na vifo.

Wamarekani walikuwa wakisherehekea siku ya shukrani ambayo huadhimishwa kila alhamisi ya nne ya mwezi Novemba kila mwaka na huwa inaendelea hadi mwishoni mwa juma.

Mwaka huu, serikali nchini humo ilikuwa imetahadharisha wananchi dhidi ya kusafiri na kuandaa sherehe kubwa ili kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya Corona.

Hata baada ya ushauri huo, mwanamuziki Cardi B aliandaa sherehe ya watu 40 wa familia yake, ambao walijumuisha watoto na watu wazima.

Mashabiki na wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii hawakufurahia jambo hilo na wengi walimkashifu. Kutokana na hayo, Cardi B aliwaomba msamaha akisema nia yake haikuwa kuudhi yeyote na kwamba alitumia hela nyingi kuhakikisha kila mmoja wa waliohudhuria amepimwa virusi vya Corona.

Kulingana naye, hiyo sherehe ya jana jumapili ndio ilikuwa nafasi ya kwanza ya kuwa na watu wote wa familia yake nyumbani kwake jambo alisema liliridhisha moyo wake.

Baada ya kuomba msamaha, Cardi B tena aliandika “Watu wanajikaza sana kukasirikia vitendo vyangu. Nashangaa wanamudu vipi maisha kwenye ulimwengu halisi.”

Sio mara ya kwanza Cardi analazimika kuomba msamaha kwenye mitandao ya kijamii, kuna wakati aliomba msamaha baada ya kuleta dhana ya mungu wa kike wa dini ya Hindu kwenye picha ya mauzo ya viatu vyake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *