Pande hasimu zasababisha ghasia katika bunge la kaunti ya Nyandarua

Vurugu zilizuka Jumanne alasiri katika bunge la kaunti ya Nyandarua baada ya kundi la wanaume waliokuwa wamevalia suti nyeusi kuvamia bunge hilo na kujaribu kutwaa mesi ya spika.

Juhudi za wanaume hao wenye miraba minne zilisababisha  makabiliano makali baina ya mirengo inayoegemea upande wa spika wa bunge la kaunti hiyo aliyetimuliwa Ndegwa Wahome na na upande unaoegemea gavana wa kaunti hiyo Francis Kimemia.

Wanachama wa bunge la kaunti hiyo wanaoegemea upande wa Wahome ambao wanasemekana kugadhabishwa na uamuzi wa mahakama wa kudhibitisha kufurushwa kwake, wamelaumiwa kwa kuhusika na vurugu hiyo.

Kisa hicho kilitokea muda mfupi tu baada ya kaunti hiyo kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka wa 2020. Baada ya makabiliano ya dakika 30, polisi waliingilia kati na kumkamata mwakilishi wa wodi ya Gatimu Kieru Wambui ambaye ni mshirika wa karibu wa Wahome.

Kiongozi wa walio wengi katika bunge la kaunti hilo  Ednard King’ori alidhibitisha kuwa aliwafahamisha polisi kuhusu hatua ya wanaume hao waliokuwa wamevalia suti nyeusi ya kuvamia bunge la kaunti hiyo mwendo wa saa nane na nusu.

Wanachama wa bunge la kaunti hiyo wanaoegemea upande wa gavana Kimemia wameazimia kukita kambi katika bunge la kaunti hiyo na kuhakikisha kuwa polisi wanalinda mesi hiyo.

Mahakama moja ya Nakuru ilikuwa imedumisha kufurushwa kwa Wahome ambaye pia ni mwenyekiti wa kongamano la mabunge ya kaunti nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *