Oparanya ajitosa kupigania tiketi ya ODM ili kuwania urais mwaka wa 2022

Gavana wa Kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya ameelezea matumaini ya kupata tiketi ya chama hicho ili kuwania urais mwaka wa 2022.

Oparanya, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini, amesema atatuma ombi la kuteuliwa ili kujiunga na wale watakaopigania tiketi ya chama hicho ya kuwania urais.

Tayari chama cha ODM kimewataka wanachama wake kutuma maombi kwa bodi ya kitaifa ya uchaguzi ikiwa wanataka kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho kwenye uchaguzi wa urais wa mwaka 2022.

Chama hicho kimesema kuwa wanaotaka kuwania uteuzi huo sharti walipe ada ya shilingi milioni moja kwa akaunti ya benki ya chama hicho.

Ili mgombea kufaulu kuwania kiti hicho, ni sharti awe Mkenya ambaye ameejisajili kama mpiga kura na pia awe mwanachama wa kudumu wa chama cha ODM na aliyehitimu shahada ya kutoka chuo kikuu chochote kinachotambulika.

Aidha, atahitajika kuwa na vigezo vinavyohitajika kwa wagombea urais jinsi ilivyoratibiwa na Tume Huru ya uchaguzi na mipaka nchini (IEBC).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *