Ommy Dimpoz kujiunga na Sony Music Africa

Mwanamuziki wa nchi ya Tanzania Ommy Dimpoz kwa jina halisi Omary Nyembo atajiunga rasmi na kampuni ya kimataifa ya muziki kwa jina Sony Music Africa kesho.

Habari kuhusu hatua hiyo ya Ommy Dimpoz zilijulikanishwa na meneja wake mmiliki wa kampuni ya muziki nchini Tanzania inayoitwa “Rockstar Africa” mwanadada Seven Mosha.

Mosha aliongeza tena kwamba Ommy Dimpoz atazindua albamu ya kwanza mwakani lakini hivi leo mnamo saa kumi jioni atazindua kibao kipya kwa jina, “Dede”.

Ommy Dimpoz amekuwa kwenye ulingo wa muziki nchini Tanzania kwa muda sasa na anajulikana kwa vibao kama vile, “Tupogo”, “Nai Nai” na vingine.

Alianza kuimba mwaka 2005 akiwa shule ya upili pale alipoanzisha kundi kwa jina “West VIP”. Aliimba pia katika kundi jingine kwa jina “Top Band” hadi mwaka 2011 alipoamua kuimba peke yake.

Wimbo wake wa kwanza ‘Nai Nai’ uliwahi kuteuliwa na kushinda kwenye tuzo kadhaa hata zile za Kenya kwa jina ‘Nzumari”.

Ameshirikisha wanamuziki wengine tajika katika kazi yake kama vile Christian Bella, Dully Sykes na Avril wa Kenya kati ya wengine wengi.

Mwaka 2018 afya yake ilidhoofika ikasemekana kwamba alikuwa anaugua saratani akaja Kenya kutafuta matibabu kisha akaelekezwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Alipohojiwa baada ya kupona, alisema kwamba Gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho aligharamia kikamilifu matibabu yake.

Mwanamuziki wa Tanzania Ali Kiba pia yuko chini ya hiyo lebo ya kimataifa ya Sony.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *