Olunga atawazwa mfungaji bora ligi kuu Japan kwa kupiga bao la 27

Mshambulizi wa Harambee Stars Michael   Olunga  amejihakikishia kunyakua tuzo ya mfungaji bora katika ligi kuu  nchini Japan  msimu huu, baada ya kupachika bao la 27 Jumatano adhuhuri na kuisaidia timu yake ya Kashiwa Reysol kuibwaga Sanfrece Hiroshima bao 1-0 ugenini .

Olunga alipachika bao hilo katika dakika ya 17 baada ya kuunganisha pasi ya mshambulizi Hiroto Gaya  na kufyatua tobwe la chini pembeni kulia kutoka ndani ya hatua ya miguu 18 na matokeo hayo kusimama hadi kipenga cha mwisho.

Bao hilo lilimwezesha Engieneer Olunga kusawazisha rekodi ya mabao 27 aliyofunga msimu jana akiwa na timu hiyo katika ligi ya daraja ya kwanza nchini Japan na kumaliza wa pili katika ufungaji mabao,ingawa msimu huu tayari ametwaa tuzo hiyo ya kiatu cha dhahabu kwani  amemwacha mfungaji wa pili bora Everaldo kutoka Kashima Antlers  kwa magoli 10 ikisalia mechi moja msimu ukamilike  .

Kwa jumla Kashiwa imefunga mabao 58 msimu huu katika ligi kuu ,27 kati yake yakifungwa na Olunga ambaye amekuwa na msimu wa kwanza wa  kufana .

Ligi hiyo itakamilika Jumamosi Disemba 19 kwa michuano ya awamu ya 34 ambapo  Kashiwa yake Olunga itakuwa nyumbani dhidi ya mabingwa Kawasaki Frontale.

Hata hivyo Kashiwa tayari imepoteza nafasi ya kufuzu kwa ligi ya mabingwa barani Asia ikiwa ya 7 kwa pointi 52.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *