Categories
Michezo

Olunga alenga kuandikisha historia kucheza FIFA World Cup

Mshambulizi  wa Harambee Stars Michale Olunga anatarajiwa kuingia kwenye madaftari ya kumbukumbu kuwa Mkenya wa kwanza kucheza mashindano ya kombe la dunia baina ya vilabu yatakayoanza  Alhamisi hii nchini Qatar.

Olunga aliye na umri wa miaka 26 amejumuishwa kwenye kikosi cha klabu ya Al Duhail Sc  huku wakicheza mchuano wa ufunguzi Alhamisi Februari 4 dhidi ya mabingwa wa Afrika Al Ahly kutoka Misri.

Awali Mc Donald Mariga alikuwa kwenye kikosi cha Inter Milan ya Italia kilichonyakua kombe la dunia mwaka 2010 katika muungano wa Milki za kiarabu.

Olunga ambaye aliibuka mfungaji na mchezaji bora katika ligi kuu ya Japan mwaka jana akiwa na klabu ya Kashiwa Reysol alijiunga na mabingwa hao wa Qatar kwa kima cha shilingi milioni 933 ambapo anakisiwa kulipwa mara dufu ya mshahara aliokuwa akilipwa akiwa Japan .

Mshambulizi huyo wa Kenya anatarajiwa kuichezea Al Duhail katika mechi ya robo fainali ya kombe la dunia Alhamisi dhidi ya mabingwa mara 9 wa Afrika Al Ahly baada ya kujumuishwa kwenye kikosi cha wanandinga 23 wa mabingwa hao watetezi wa ligi kuu Qatar zamani wakifahamika kama Lakhwiya.

Katika mechi nyingine ya robo fainali ya Alhamisi mabingwa wa Marekani kaskazini Tigres UNL  ya Mexico itapambana na mabingwa wa bara Asia Ulsan Hyundai.

Mashindano ya kombe la dunia kati ya vilabu yanajumuisha mabingwa wa kila bara ,Ulaya ikiwakilishwa na Bayern munich na Palmeiras wakiwakilisha Marekani Kusini  huku fainali yake ikisakatwa Februari 11.

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *