ODM yashinikizwa kuandaa uteuzi wa mgombea wa uchaguzi mdogo wa Bonchari

Mwaniaji mmoja kwenye uchaguzi mdogo wa Eneo Bunge la Bonchari ameibua wasiwasi kuhusiana na chama cha ODM kutotoa kauli yoyote kuhusiana na uteuzi wa chama hicho.

David Ogega, anayenuia kuwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha ODM, ameihimiza kamati kuu ya chama hicho kuzungumzia uteuzi wa uchaguzi huo mdogo ili wawaniaji wajiandae.

Akiwahutubia wanahabari katika Kaunti ya Kisii, Ogega alisema kiongozi wa chama hicho Raila Odinga anafaa kuhakikisha kwamba uteuzi huo unafanyika kwa njia yenye uwazi.

Akiandamana na baadhi ya wanachama wa ODM, Ogega alidai kwamba baadhi ya wawaniaji wanataka uteuzi wa moja kwa moja wa mwaniaji wa chama hicho.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa tawi la chama cha walimu, KNUT, katika eneo la Kisii kusini, Geoffrey Mogire, aliyekuwa meneja wa tawi la Kisii la Benki ya Kenya Commercial, John Billy Momanyi, na aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Zebedeo Opore ni miongoni mwa wale walioelezea nia ya kuwania kiti hicho.

Ni kilti kilichoachwa wazi kufuatia kifo cha Mbunge wa eneo hilo John Oroo Oyioka.

Uchaguzi huo mdogo wa Bonchari utaandaliwa tarehe 18 mwezi Mei mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *