Nyota 21 – T.I.D

Msanii wa muziki nchini Tanzania Top In Dar es salaam maarufu kama T.I.D anasherehekea miaka 21 tangu aanze kazi ya muziki wa Bongo.

Katika kuadhimisha miaka hiyo 21 ya kuburudisha wengi ndani na nje ya Tanzania, T.I.D amepanga mengi tu na moja kati ya mambo hayo, ni filamu kuhusu maisha yake katika muziki.

Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Khaled Mohamed ni mmoja kati ya wasanii walioanzisha muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania.

Kitu kingine ambacho amekipanga ni ziara katika sehemu mbali mbali za Tanzania kuanzia Dodoma tarehe 27 mwezi huu wa Februari mwaka 2021 na atakuwa akisindikiwa na wasanii kama vile G Nako, Lulu Diva, Linah, Domo Kaya na Sholo Mwamba.

Tukio hilo litaandaliwa huko Royal Village kuanzia saa moja jioni.

Atazuru pia mikoa mingine kama Mwanza, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam.

Vibao vyake vya awali kama vile “Zeze” na “Siamini” viliwika sana nyakati hizo ndani na nje ya Tanzania.

T.I.D wa umri wa miaka 40 sasa, alizindua ziara hii ya Nyota 21 jana kwenye kikao na wanahabari katika hoteli ya Regency Park Jijini Dar Es Salaam.

Angehojiwa hiyo jana jioni kwenye kipindi kwa jina “Trafik Jamz” cha kituo cha redio cha Clouds lakini akatoa tangazo kwenye akaunti yake ya Instagram akisema kwamba mahojiano hayo yameahirishwa bila kutoa sababu.

T.I.D ameingilia pia uigizaji na anaigiza kama Kenzo kwenye kipindi kiitwacho “Jua Kali” ambacho huonyeshwa kwenye Maisha Magic Bongo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *