Nkechi Blessing na Bobrisky warushiana maneno

Wawili hao ni maarufu nchini Nigeria, Nkechi kutokana na uigizaji kwenye filamu za Nollywood na Bobrisky kutokana na hatua yake ya kuamua kuvaa na kuishi kama mwanamke ilhali alizaliwa mwanaume.

Tatizo lilianza wakati Bobrisky au ukipenda Okuneye Idris alipata mahali ambapo Nkechi Blessing Sunday amemtaja na kumrejelea kama hayawani kuhusiana na kioja kinachoendelea cha mashabiki kuchora “Tatoo” zao.

Bobrisky alimsuta Nkechi huku akisema kwamba yeye hufurahia amani hata kwenye mitandao ya kijamii na kwa kumtaja alikuwa anaamsha joka.

Kulingana naye muigizaji huyo anatumia jina lake kujitafutia umaarufu kwenye mitandao ya kijamii na ikiwa anataka amani asiwahi taja jina lake tena.

Alimtaka muigizaji huyo kumwomba msamaha moja kwa moja ikiwa zogo lao ni la kwisha ingawaje hakutaja hatua ambayo angechukua ikiwa hangeombwa msamaha.

Bobrisky ambaye ana mazoea ya kugawia mashabiki wake sugu hela, alimtaja Blessing kuwa mtu asiye na utajiri wa kutosha ili kuwashukuru mashabiki wake kwa zawadi ghali anavyofanya yeye.

Nkechi ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani,alikataa kujibu shutuma hizo za Bobrisky lakini baadaye akaamua kumjibu kupitia Insta Stories.

Haijulikani ugomvi wa wawili hao utaishia wapi lakini ni burudani kwa mashabiki wao kwenye Instagram.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *