Nilidhani nitakufa, Wema Sepetu

Mwanamitindo na muigizaji maarufu nchini Tanzania Bi. Wema Sepetu amezungumzia maradhi aliyougua kwa mara ya kwanza kabisa kwenye mahojiano na gazeti moja nchini Tanzania.

Wema ambaye pia hujiita “The Tanzanian Sweetheart” alifichua kwamba amekuwa akiugua homa ya mapafu au ukipenda “Pneumonia” ambayo ilisababisha kifua chake kijae na ikawa vigumu kwake kupumua.

Alisema kwa wakati mmoja alikuwa na maumivu makali mpaka akadhani kwamba ni kifo kinamjia. Wema ambaye anaendelea kupona anasema akipona kabisa atasema dua kwa mwenyezi Mungu kumshukuru kwa kulinda maisha yake.

Afya ya muigizaji huyo ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mpenzi wa Diamond Platnumz imekuwa ikitiliwa shaka na mashabiki wake ndani na nje ya Tanzania hasa baada yake kupunguza kwa kiasi kikubwa uzani wa mwili.

Ombi lake kwa mashabiki wake kwa sasa ni kwamba waendelee kumwombea ili apone kabisa kwani ugonjwa huo wake huwa unajirudia mara kwa mara.

Anaonekana kujikaza sana maanake kupitia Instagram, ametangaza kwamba amechapisha kipindi kipya cha upishi kwenye “App” yake kwa jina ‘Wema App’.

Sio siri kwamba binti huyo ambaye wakati mmoja alishinda shindano la ulimbwende na kuiwakilisha Tanzania kama “Miss Tanzania” amekuwa akitaka sana kupata mtoto lakini tatizo la afya ambalo hakufichua limemzuia.

Maajuzi amezua minong’ono kwenye mitandao ya kijamii baada ya kununua mbwa wa rangi nyeupe akampa jina, “Vanilla Nunu” na akamfungulia akaunti ya Instagram ambayo kufikia sasa ina wafuasi zaidi ya elfu 12.

Maelezo kwenye akaunti ya Vanilla Nunu yanasema, “Mimi ndiye mbwa mwenye raha kabisa unayemjua. Mamangu ni mpenzi wa Tanzania Wema Sepetu. Karibu kwa ulimwengu wangu. Na ndio mimi nimeharibiwa sana angalau hilo ndilo mamangu hunifanyia.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *