Categories
Habari

Ngilu amkemea Ruto kwa kudai kwamba Kalonzo alinyakua ardhi ya Yatta

Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu amemtetea vikali kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka dhidi ya madai ya Naibu Rais William Ruto kwamba alijipatia ardhi ya Yatta kwa njia isiyo halali.

Kulingana na Ngilu, madai ya wizi wa shamba dhidi ya Kalonzo hayana ukweli wowote na yanalenga kumchafulia sifa.

Ngilu, aliyehudumu kama Waziri wa Ardhi wakati wa kipindi cha kwanza cha Rais Uhuru Kenyatta, amesisitiza kwamba ardhi hiyo ya Yatta ni ya Kalonzo na aliipata kwa njia halali.

“Kama Waziri wa Ardhi, nilitazama maelezo kuhusu kipande hicho cha ardhi na naweza kuthibitisha kwamba Kalonzo alikipata kwa njia halali kabisa,” akasema Ngilu.

Amesema ameshangazwa sana na hatua ya Naibu Rais William Ruto kutoa madai hayo wakati huu dhidi ya aliyekuwa Makamo wa Rais Kalonzo Musyoka.

Kulingana na Gavana Ngilu, matamshi ya Ruto yanalenga kujiepusha na macho ya umma kwa vile anakabiliwa na madai ya kufanana na hayo, akihoji kwamba Naibu Rais huyo ametajwa kwenye kesi nyingi za unyakuzi wa ardhi.

“Nafikiri kila Mkenya anajua. Nilipokuwa Waziri wa Ardhi, nilimshuhudia Ruto akijaribu kunyakua ardhi ya Shule ya Msingi ya Langata iliyoko karibu na Hoteli yake ya Weston,” akasema.

Ngilu amesema kwamba ilimlazimu Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati sakata hiyo na hatimaye ardhi hiyo ikazungushiwa ua na kumilikiwa kikamilifu na shule hiyo.

Wakati uo huo, gavana huyo amemkashifu Naibu Rais kuhusu kampeni yake ya walala hoi, akihoji kwamba kampeni hiyo haitaleta chochote cha maana.

“Hawezi kuwahadaa vijana kwamba anawasaidia wakati amekuwa uongozini kwa karibia miaka 30 na sasa anaanza kuwanunulia mikokoteni,” akaongeza Ngilu.

Amesema vijana wanahitaji kuwezeshwa kwa njia mwafaka ndipo wafanikiwe kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *