Ngatia: Uhusiano wangu na Rais Kenyatta hautahujumu uhuru wa Mahakama

Wakili Fred Ngatia amepuuziilia mbali hofu kwamba uhusiano wake wa karibu na Rais Uhuru Kenyatta unaweza kutatiza uhuru wa idara ya mahakama, endapo atachaguliwa jaji mkuu kumrithi David Maraga aliyestaafu.

Ngatia mwenye umri wa miaka 65, ambaye mara mbili alimwakilisha Rais Uhuru Kenyatta kwenye rufaa zilizowasilishwa na Raila Odinga dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais mwaka wa 2013 na 2017, aliliambia jopo la tume ya idara ya mahakama ingawaje anafurahia kumwakilisha kiongozi wa nchi, uhusiano wao ulikamilika baada ya kesi hizo na akarejelea kazi yake ya kibinafsi ya uwakili.

Wakili huyo alitoa wito kwa tume hiyo isimbague kwa kumwakilisha kiongozi wa nchi ambaye alikuwa mteja wake sawa na mteja mwingine wowote ambaye amewakilisha katika taaluma yake ya miongo minne.

“Msinibague kwa sababu ya mteja yeyote niliyehudumia. Nimewakilisha matajiri na masikini. Rais sawia na mkenya yeyote alihitaji huduma za wakali, sioni haya kumhudumia,” alisema Ngatia

Ngatia alisema akiteuliwa kuwa jaji mkuu mpya wa Jamhuri ya Kenya, atajizatiti kukita maadili miongoni mwa maafisa wa idara ya mahakama ili kutokomeza ufisadi katika idara hiyo.

Jaji William Ouko anatarajiwa kufika mbele ya tume hiyo Jumatano kabla ya tume hiyo kuwasaili Profesa Moni Wekesa na Alice Yano siku ya Alhamisi na ijumaa mtawalia.

Baada ya kukamilisha usaili tume hiyo inahitajika kuwasilisha majina ya waliofaulu kwa rais katika muda wa siku saba.

Rais kisha anatarajiwa kuwasilisha jina bungeni kwa usaili na uidhinishaji. Iwapo bunge litakatalia mbali aliyependekezwa, tume ya idara ya mahakama itaanzisha upya shughuli ya usaili. 

Iwapo bunge litaidhinisha aliyependelezwa, rais atamteuwa rasmi kuwa jaji mkuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *