NEMA yasimamisha mradi wa Mzuri Sweets wa mabilioni ya pesa huko Kilifi

Mradi wa uwekezaji wa mabilioni ya fedha katika eneo la Kwa Kadzengo, Kaunti ya Kilifi  umesimamishwa na Halmashauri ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingiria (NEMA) kwa madai ya kuvamia eneo chemichemi.

Mradi huo unaojulikana kama Mzuri Sweets, ulikuwa umeidhinishwa na asasi husika za serikali lakini NEMA imeusimamisha kwa muda usiojulikana.

Kulingana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo John Konchella, uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwa  sehemu ya bohari linalojengwa imeingia umbali wa mita 30 katika eneo la chemichemi.

“Ufukiaji wa chemichemi kwenye ardhi nambari LR531 umeendelea licha ya mtekelezaji wa mradi huo kupewa agizo la kusitisha zoezi hilo mnano tarehe 15 Aprili, 2020,” akasema Konchella.

Mhandisi Zephania Ouma ambaye ni Kaimu Mkrugenzi wa uafikiaji na utekelezaji wa kanuni kwenye  halmashauri hiyo ameeleza sababu ya kusimamisha mradi  huo ambao awali walikuwa wameuidhinisha.

Amedokeza kuwa ripoti ya uchunguzi wa athari ya mradi huo kwa mazingira haikutimiza masharti yaliowekwa.

Hata hivyo, wasimamizi wa Mzuri Sweets wamepinga hatua ya kusimamishwa kwa ujenzi wa mradi huo wakikariri kuwa ulikuwa umekamilika kwa asilimia 80 na kwamba walitimiza masharti yote ya uchunguzi wa athari ya mradi huo kwa mazingira na kuidhinishwa na mamlaka zote husika.

Huu ni mradi wa pili mkuu katika Kaunti ya Kilifi kusimamishwa na NEMA mwaka huu baada ya halmashauri hiyo kudinda kuidhinisha ripoti ya tathmini ya athari za kimazingira ya ujenzi wa hoteli huko Watamu.

Hoteli hiyo ya ghorofa 60 kwa jina Palm Exotica ulikuwa umepangwa kugharimu shilingi bilioni 23.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *