NCIC yapinga ufufuzi wa kesi za ghasia za baada ya uchaguzi

Tume ya Utangamanio na Uwiano wa Kitaifa, NCIC, imeonya kwamba jaribio lolote la kutaka kufufua tena kesi za ghasia za baada ya uchaguzi huenda likasababisha machafuko mapya humu nchini.

Tume hiyo imeeleza kuwa jamii zilizohusika kwenye ghasia hizo zilizosababisha maafa na Wakenya wengi kupoteza makao yao zinaonekana kuwa zimesameheana.

Haya yanajiri siku moja baada ya Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai George Kinoti kufafanua kwamba idara hiyo hailengi kufufua tena kesi zilizoamuliwa tayari.

Jumatatu, Kinoti aliwahutubia waathiriwa wa ghasia hizo na kusema kwamba DCI iko tayari kuwafungulia mashtaka waliohusika katika kupanga na kutekeleza ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Hatua hiyo iliibua hisia na lalama kutoka kwa viongozi mbali mbali hasa wale wa eneo la Bonde la Ufa.

Mwenyekiti wa NCIC Dkt. Samuel Kobia amesifu ufafanuzi wa Kinoti akihoji kwamba taarifa yake ya Jumatatu ilikuwa imeibua wasi wasi mwingi miongoni mwa Wakenya.

“Waathiriwa wanakubali kwamba walipitia uchungu mwingi lakini sasa wamepona na kusameheana kwa hivyo hakuna haja ya kurejelea maswala hayo tena,” akasema Dkt. Kobia.

Kobia ameeleza kuwa tume ya NCIC inalenga kuhimiza amani na msamaha unaodhihirishwa na jamii zilizoathirika kwenye mapigano hayo machafu.

“Nchi hii inapojiandaa kwa kura ya marekebisho ya katiba, tunafuatilia kwa umakini sana kuhakikisha kwamba maswala tisa yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya BBI yanatekelezwa,” akasema.

Dkt. Kobia amesema haya kwenye mkutano na maafisa wa usalama kutoka Kaunti za Narok na Nakuru, ambapo ametaja mzozo wa ardhi na wizi wa mifugo kama baadhi ya changamoto zinazokumba jamii hizo mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *