Nandy aangukia ubalozi wa sodo

Mwanamuziki wa Tanzania Nandy ambaye hujiita ‘The African Princess’ sasa ndiye balozi wa sodo za chapa ya “Flowless” ambazo zinapatikana kwa soko la Tanzania.

Tangazo hilo lilitolewa jana alhamisi na kampuni ya kuunda sodo hizo kwa kikao na wanahabari ambapo Nandy alikuwa na akatia saini makubaliano ya kazi hiyo ya ubalozi.

Sio mara ya kwanza kwa Nandy kufanya kazi na kampuni hiyo ya kuunda pedi za Flowless kwani mwaka jana yapata mwezi wa tano, picha yake ilitumika kwenye mabango ya mauzo ya pedi hizo.

Akizungumza baada ya kutia saini makubaliano hayo, Nandy alisifia sodo hizo akisema mwanamke anayezitumia anaweza kufanya jambo lolote bila kuogopa wakati wa hedhi.

Wasimamizi wa kampuni hiyo walisema walimchagua Nandy kwa sababu ni mwanamke ambaye anajiamini, jasiri na ambaye hakati tamaa maishani.

Alijipatia fursa hiyo pia kwa jinsi amekuwa akijulikanisha ujio wa pedi hizo ambazo zilizinduliwa rasmi mwaka jana 2020.

Nandy pia anaendeleza kazi nyingine kama hiyo kwa bidhaa ya sabuni kutoka kwa kampuni inayojulikana kama Azania. Ameonekana kwenye picha za mauzo za sabuni hiyo ya unga kwa jina King Limau.

Nandy ambaye jina halisi ni Faustina Charles Mfinaga, alizaliwa mwezi Novemba mwaka 1992 nchini Tanzania na alianza rasmi kazi ya muziki mwaka 2013.

Kazi hii yake imewadia wakati mashabiki wake wanasubiria kwa hamu kazi ya muziki kutoka kwake kwa ushirikiano na Koffi Olomide wa Congo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *