Mwilu ataka vikao vya mahakama virejelewe kikamilifu

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu amedokeza kuhusu uwezekano wa kurejelewa kwa shughuli za kawaida katika huduma za mahakama kote nchini.

Akiongea wakati wa kikao cha kila mwaka cha majaji wa mahakama kuu katika Kaunti ya Mombasa, Mwilu alisema kuwa mahakama haziwezi kusalia kufungwa na vikao vya kawaida kukosa kuendelea kwa muda mrefu.

Mwilu alisema kuwa watumizi wa mahakama wamewashtumu majaji kwa kukosa kuandaa vikao kwa njia ipasayo, kwa vile mashahidi hawasikizwi.

“Mashahidi hawapati fursa ya kusikizwa katika vikao vingi vya mahakama vya moja kwa moja wala kupitia mtandao. Tutaendelea kujifungia mpaka lini hali sehemu zengine zimefunguliwa?” akasema Mwilu.

Kwa sasa vikao vya moja kwa moja vya mahakama huhudhuriwa na watu wachache tu kwa kuzingatia janga la korona, lakini Mwilu anasema ni wakati kanuni hizo zifanyiwe mabadiliko ili kuhakikisha kunakuwa na utoaji wa haki ulio sawa sawa.

Alisema kuwa idara ya mahakama imejitolea kuhakikisha kuwa wafanyikazi wake na watumizi wote wa mahakama wako salama kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa kudhibiti virusi vya korona.

Idara ya mahakama ilipunguza shughuli zake baada ya kuzuka kwa janga la korona mwezi Machi mwaka jana.

Takwimu zinaonyesha kwamba mwaka wa 2020, jumla ya kesi 10,646 zilisajiliwa katika mahakama mbali mbali humu nchini lakini ni kesi 7,713 tu zilizotatuliwa.

Kufikia mwezi Juni mwaka huo, kulikuwa na jumla ya kesi 89,415 ambazo hazijaamuliwa katika mahakama kuu, idadi ambayo iliongezeka hadi 92,530 kufikia mwisho wa mwaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *