Mwili wa waziri wa zamani Joe Nyaga kusitiriwa Jumamosi

Mazishi ya mwanasiasa mkongwe Joe Nyaga yatafanyika Jumamosi nyumbani kwake Kamutungi katika Kaunti ya Embu.

Tarehe hiyo ya mazishi imeafikiwa kwenye kikao baina ya familia yake, jamaa, marafiki na viongozi wa kidini.

Kulingana na kaka yake Norman Nyaga, ibada ya mazishi hayo itaongozwa na Askofu Joel Waweru wa Kanisa la ACK Nairobi.

Mwili wa marehemu Nyaga utasitiriwa karibu na makaburi ya wazazi wake, babu yake na kaka yake Zachariah.

Familia hiyo imeeleza kwamba Nyaga alifariki kutokana na makali ya ugonjwa wa COVID-19 ulioharibu pafu zake kwa asilimia 97.7, na kusisitiza kwamba kanuni za kuzuia msambao huo zitazingatiwa vilivyo wakati wa mazishi hayo.

Alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi cha Hospitali ya Nairobi mnamo tarehe 17 Novemba hadi tarehe 11 Desemba alipoaga dunia.

Joe Nyaga ni mwanawe Jeremiah Nyagah ambaye alikuwa waziri katika serikali ya Hayati Mzee Jomo Kenyatta na pia aliyepigania uhuru wa taifa hili.

Joe Nyaga alichaguliwa Waziri wa Maendeleo ya Ushirika katika serikali ya mseto baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.

Mwaka wa 2017, Nyaga alijiuzulu kama mshauri wa Rais Uhuru Kenyatta na kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais kama mwaniaji wa kibinafsi.

Alikuwa mwanachama wa kundi la ‘Pentagon’ la chama cha ODM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Nyaga awali alikuwa mbunge wa Gachoka ambayo sasa ni Mbeere kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *