Mwili wa Nyachae wawasili Kisii kwa ajili ya mazishi Jumatatu

Mwili wa aliyekuwa Waziri Simeon Nyachae umewasili Kisii kwa matayarisho ya hafla ya mazishi itakayofanyika Jumatatu katika Uwanja wa Gusii.

Ndege ya polisi iliyokuwa imebeba mwili huo imetua katika uwanja wa Shule ya Kisii aliyosomea Nyacha kabla kupelekwa nyumbani kwake.

Viongozi mbali mbali wa kaunti hiyo wamepokea jeneza lililokuwa na mwili wa Nyachae japo hawakupata nafasi ya kuutazama mwili wenyewe.

Haya yanajiri huku usalama ukizidi kuimarishwa katika Mji wa Kisii na vile vile katika boma la marehemu, eneo la Nyosia.

Kamishna wa Kaunti ya Kisii Allan Macharia amefichua kwamba watu wapatao elfu kumi wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo Jumatatu huku mipango ya kudhibiti usafiri kwenye barabara za eneo hilo ukiwa umekamilika.

Macharia ameusihi umma kushirikiana na polisi wa trafiki hasa katikati ya mji wa Kisii ili kuwe na utaratibu ufaao wa usafiri wa magari na pia wanaoenda kwa miguu.

Kamishna huyo pia amethibitisha kwamba serikali itasisitiza kuzingatiwa kwa kanuni za kuzuia msambao wa virusi vya korona, ikiwemo watu kutokaribiana, kunawa mikono na kuvaa barakoa wakati wa hafla hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *