Mwenyekiti wa shirika la KBC David Were aifariji familia ya marehemu Justus Murunga

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa shirika la utangazaji nchini-KBC David Were alizuru makazi ya aliyekuwa mbunge wa Matungu marehemu Justus Murunga katika eneo la Embakasi jijini Nairobi ili kuifariji familia yake.

Were ambaye alikuwa ameandamana na mkewe, alitoa wito kwa wakazi wa eneo bunge la Matungu kusalia watulivu na kuungana na familia ya marehemu katika maombi wakati huu wa majonzi.

Were ambaye ni mbunge wa zamani wa  Matungu, alipoteza kiti hicho mwaka wa 2017.

Siku ya alhamisi hakimu wa mahakama ya  Milimani Agnes Makau alitoa maagizo ya kusimamisha mazishi ya marehemu mbunge huyo wa Matungu.

Hii ni baada ya mwanamke mmoja kwenda mahakamani akidai kuwa alizaa watoto na mbunge huyo.

Mahakama ilimwagiza mwanamke huyo kwa jina Agnes Wangui kuwakabidhi wake wawili wa mbunge huyo na hifadhi ya maiti ya Lee Funeral stakabadhi za mahakama kabla ya kesi hiyo kusikizwa tarehe 26 mwezi huu.

Wangui kupitia kwa wakili  Danstan Omari alikuwa anataka wajane wawili wa marehemu Christabel na  Grace na hifadhi ya maiti ya Lee kusimamishwa kufanya mipango yote ya mazishi.

Wangui pia alitaka kuchukuliwa kwa sampuli za  DNA kutoka kwa marehemu na watoto wake ili kubaini wazazi wao halisi.

Anataka mwili wa marehemu kuhifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya  Lee hadi sampuli za DNA zichukuliwe mbele ya mpasuaji wa maiti aliyeidhinishwa atakayeteuliwa na pande hizo mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *