Mwendelezo la Black Panther

Kampuni ya kutayarisha filamu ya Marekani “Marvel Studios” imetangaza jina la mwendelezo wa filamu iliyopendwa sana ya mwaka 2018 kwa jina “Black Panther”.

Filamu ya kuendeleza hadithi hiyo itafahamika kama “Black Panther: Wakanda Forever” na itazinduliwa rasmi tarehe 8 mwezi Julai mwaka ujao wa 2022.

Kampuni ya Marvel haijafichua mengi kuhusu utayarishaji wa mwendelezo huo lakini kinachojulikana ni kwamba Ryan Coogler anarejea katika nafasi yake kama mwandishi na mwelekezi.

Waigizaji Letitia Wright aliyeigiza kama Shuri, Winston Duke aliyeigiza kama M’Baku, Lupita Nyong’o aliyeigiza kama Nakia na Angela Bassett ambaye aliigiza kama Queen Ramonda wote wametia saini mkataba wa kuendeleza majukumu yao kwenye filamu hiyo.

Mhusika mkuu kwa filamu ya Black Panther King T’Challa, jukumu lililoigizwa na marehemu Chadwick Boseman aligusa nyoyo za wengi ulimwenguni.

Boseman aliigiza vyema kabisa mpaka kampuni ya Marvel inakusudia kutotafuta wa kuigiza katika nafasi hiyo baada ya kifo chake na hivyo kumaliza nafasi hiyo.

Lakini mashabiki wanapigania sana uwepo wa mhusika huyo katika mwendelezo wa filamu ya Black Panther maanake ndiye shujaa mkubwa wa kwanza mweusi kwenye ulingo wa filamu.

Kwa sababu hiyo, mashabiki walianzisha ombi kwenye mitandao kwa kampuni ya Marvel kutotupilia mbali nafasi ya mfalme T’challa na ombi hilo limetiwa saini na watu wengi.

Chadwick Boseman aliaga dunia mwezi Agosti mwaka 2020 baada ya kuugua saratani ya utumbo kwa muda. Haijulikani ni hatua gani waandalizi wa filamu hiyo watachukua kuhusiana na mhusika “King T’challa” wanapoandaa mwendelezo wa “Black Panther”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *