Mwanzilishi wa onyo kwa ulimwengu dhidi ya kukopesha Kenya afunguliwa mashtaka

Mwanaharakati aliyetengeneza ilani ya kuuonya ulimwengu dhidi ya kutoa mikopo ya kifedha kwa serikali ya Kenya amefikishwa mahakamani.

Edwin Mutemi Kiama alikamatwa siku ya Jumanne kwa tuhuma za kukiuka sheria ya matumizi ya tarakilishi na uhalifu wa mtandao ya mwaka wa 2018.

Kulingana na stakabadhi za mashtaka dhidi yake, Kiama alichapisha kwenye mtandao wake wa Twitter, habari za ilani kwa ulimwengu kwamba Rais Uhuru Kenyatta hafai kufanya biashara kwa niaba ya nchi hii na kwamba hata vizazi vijavyo havitajukumika na kulipa riba na mikopo inayoombwa na Rais.

Wapelelezi wamesema kwamba habari hizo zilizochapishwa kwenye akaunti ya Twitter ya Mwarimu Wa Kiama and Wanjiku Revolution ni chapisho la uongo na ni kinyume cha sheria.

Wakati ya kukamatwa kwake, mshukiwa huyo alipatikana na vipakatalishi vitatu, simu mbili na vifaa vyengine vya kielektroniki ambavyo vilichukuliwa na kupelekwa kwa maabara ya kidijitali ili vifanyiwe uchunguzi zaidi.

Maafisa wa upelelezi pia wanawasaka watu wengine wanaoaminika kushirikiana na Kiama kuchapisha ujumbe huo.

Haya yanajiri baada ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kufichua kwamba limeidhinisha mkopo wa shilingi bilioni 255 kwa taifa la Kenya, mkopo unaotarajiwa kulipwa kwa muda wa miaka mitatu.

Kufuatia habari hizo, baadhi ya Wakenya walivamia mitandao ya kijamii ya IMF na kuishtumu bodi hiyo kwa kile walichokitaja kuwa kuendelea kutoa mikopo ilhali hakuna uwazi kuhusu matumizi ya mikopo ya awali.

Polisi wanataka kumzuia Kiama kwa siku 14 zaidi ili kukamilisha uchunguzi wao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *