Mwanaume auawa kwa kudungwa kisu Homa Bay kufuatia ugomvi wa shilingi 50

Mwanaume mwenye umri wa miaka 23 ameuawa kufuatia ugomvi kuhusu baki ya shilingi 50, baada ya kununua pakiti ya vibanzi katika eneo la Makongeni, Mjini Homa Bay.

Dick Junior Opiyo anadaiwa kuuawa kwa kudungwa kisu wakati wa malumbano kati yake na Brian Omondi mwenye umri wa miaka 25, ambaye ni mwuzaji wa vibanzi.

Malumbano hayo yalianza baada ya Opiyo, akiwa ameandamana na rafikize wawili, kutoa shilingi 100 ili kununua pakiti ya vibanzi kwa gharama ya shilingi 50.

Kulingana na Naibu wa Chifu wa Asego, Tom Ondiek, watatu hao walijawa na gadhabu baada ya mwuzaji huyo kuchelewa kuwarudishia baki yao ya shilingi 50, hivyo basi wakaanza kuharibu duka lake.

Ondiek ameeleza kuwa mwuzaji huyo alikuwa ameenda kutafuta baki hiyo na aliporudi akakasirishwa na hatua ya wateja wake ya kuharibu duka lake.

Hapo ndipo malumbano hayo yalipoanza na mwuzaji huyo akamdunga kisu Opiyo kwenye shingo.

Opiyo alikimbizwa hadi Hospitali ya Misheni ya Mji wa Homa Bay lakini akaaga dunia wakati akipokea matibabu, baada ya kupoteza damu nyingi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Homa Bay, Sammy Koskey, amethibitisha kisa hicho na kuongeza kuwa mwuzaji huyo amekamatwa mara moja na kuzuiwa katika Kituo cha Polisi cha Homa Bay.

Koskey amesema uchunguzi umeanzishwa kuhusu kisa hicho na mshukiwa huyo atafunguliwa mashtaka baada ya uchunguzi huo kukamilika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *