Categories
Burudani

Mwanamuziki Sosuun aachana na mume wake Kenrazy

Mwanamuziki wa kike wa mtindo wa rap Sosuun ametangaza kwamba ameamua kuachana na mume wake wa miaka kumi Kenrazy ambaye pia ni mwanamuziki.

Kupitia Instagram, mwanadada huyo ambaye jina lake halisi ni Frediana Nafula anaelezea kwamba wakwe zake ndio sababu kuu ya hatua ambayo amechukua.

Kulingana naye kuna ambao hawakumpenda tangu mwanzo na walihakikisha kila mmoja katika hiyo familia pia anakosa kumpenda.

Sosuun ambaye alilelewa na mama pekee anasema hali hiyo ilisababisha wakwe kumkosea heshima na hata kumchukulia kama chokoraa.

Anasifia mama yake mzazi kwa jina Margaret ambaye anasema alijibidiisha na kuwasomesha yeye na dada zake kupitia biashara ya nguo katika soko la Gikomba.

Margaret baadaye alipata mume ambaye ni baba wa kambo wa Sosuun na hapo ndipo alifunga biashara ghafla na kuingilia unywaji pombe kiasi cha kwamba sasa anaitegemea hiyo pombe.

Frediana anasema jambo hilo pia limemletea dharau kwa watu wa familia ambayo alikuwa ameolewa ya mwanamuziki Kenrazy.

Kulingana naye sio rahisi kumlazimisha mamake aende katika kituo cha kurekebisha tabia kwa nia ya kumsaidia kuacha kutumia pombe ni mpaka akubali mwenyewe na hilo halijatimia.

Anamalizia kumwomba msamaha mpenzi wake Kenrazy kwa kutangaza mambo yao hadharani na kwa kuamua kumwacha.

Hata hivyo anakiri mapenzi yake kwa mume wake na kusema kwamba ikiwa atatafuta mpenzi katika siku zijazo atatafuta kama yeye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *