Mwanamuziki Professor Jay ashindwa kutetea kiti cha ubunge

Joseph Haule almaarufu Professor Jay mwanamuziki ambaye aliingilia siasa nchini Tanzania alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge wa eneo la Mikumi katika uchaguzi mkuu ulioganyika jumatano.

Jay wa chama cha CHADEMA alibwagwa na Dennis Lazaro wa chama cha CCM ambaye alizoa kura 31,411 na Professor Jay akapata kura 17,375.

Kiongozi wa chama chake Bwana Tundu Lissu anaonekana kutoridhishwa na shughuli nzima ya uchaguzi akisema ilikumbwa na udanganyifu kwani maajenti wake walizuiwa kuingia kwenye vituo vya kupiga na kuhesabu kura.

Haule amekuwa mbunge wa Mikumi kwa miaka mitano sasa na alishinda uchaguzi wa mwaka 2015 kupitia chama chake cha CHADEMA.

Wakati huo alijizolea kura 32,259.

Professor Jay ana umri wa miaka 44 sasa na amekuwa kwenye fani ya muziki tangu mwaka 1989 akiwa mmoja wa wasanii katika kundi la “Hard Blasters” na wakati huo alikuwa anajiita “Nigga J”.

Kundi hilo lilizindia albamu ya kwanza iliyojulikana kama “Funga Kazi” na baadaye wakaibuka washindi wa tuzo la kundi bora la muziki wa hip hop.

Alianza kuimba peke yake mwaka 2001 na kufikia sasa ana albamu sita ambazo ni “Machozi, Jasho na Damu”, “Mapinduzi Halisi”, “J.O.S.E.P.H”, “Aluta Continua”, “Izack Mangesho” na “Kazi Kazi” ya mwaka 2016 wakati akiwa mgeni bungeni.

Akiwa anahudumia watu wa Mikumi kama Mbunge, Profesor Jay alionekana kupunguza kazi ya muziki kidogo na sasa inasubiriwa kuona ikiwa atarejea kikamilifu kwenye fani hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *