Mwanamke na bintiye waokolewa kutoka kwa watekaji nyara Siaya

Washukiwa watano wamekamatwa na maafisa kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Uhalifu, DCI, huko Ugunja, Kaunti ya Siaya kufuatia kisa cha utekaji nyara wa mwanamke mmoja na bintiye.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 20 na bintiye wa miaka miwili walikuwa wakiishi kwa jamaa yao katika eneo la Sidindi kabla ya kutoweka kwa njia ya kutatanisha wiki moja iliyopita.

Maafisa hao wa upelelezi walivamia nyumba mbili mjini Luanda ambako wawili hao walikuwa wamefichwa na kuwanasa washukiwa watano.

“Watano hao wa umri wa kati ya miaka 18 na 29 wanajumuisha msichana wa miaka 18 aliyekuwa akimzuia mtoto huku mama yake akizuiliwa katika sehemu tofauti,” amesema afisa wa DCI.

Kulingana na maafisa hao, sababu za kutoroshwa kwa mama huyo na mtoto wake hazijajulikana.

Gari moja aina ya Toyota Premio lililotumika kwenye kisa hicho kilichotokea tarehe 2 Novemba lillinaswa.

Uchunguzi unaendelea kubaini ongezeko la visa vya utekaji nyara katika kaunti hiyo.

Wakati uo huo, mwanamume mmoja aliyewahi kuhudumu kama afisa wa polisi aliyekamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi huko Ruiru alifikishwa mahakamani jana kwa tuhuma za wizi wa rununu zilizodhamiriwa kuwasilishwa kama ushahidi mahakamani.

Mshukiwa huyo Moses Omondi na rafiki yake wa kike walikamatwa baada ya kufanywa msako wa kubaini kutoweka kwa rununu ambazo zingewasilishwa mahakamani kama ushahidi kwenye kesi za uhalifu.

Mwanamke huyo alipatikana na rununu ya kisasa aina ya Nokia, ambayo ingetumiwa kama ushahidi kwenye kesi inayosubiriwa kusikizwa katika mahakama ya Thika.

Afisa huyo wa polisi ambaye aliwahi kuhudumu katika afisi za Idara ya Ujasusi huko Ruiru alifutwa kazi kutokana na utovu wa nidhamu.

Omondi alikamatwa na maafisa wa polisi huko Tatu City katika Kaunti ya  Kiambu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *