Mwana Falsafa, Babu Tale, sasa ni wabunge Tanzania

Hamis Mwinjuma mwanamuziki wa mtindo wa Hip Hop nchini Tanzania almaarufu “Mwana Falsafa” au ukipenda “Mwana Fa” sasa ni Mbunge nchini Tanzania.

Atawakilisha eneo la Muheza bungeni kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Yeye ni mmoja wa watu zaidi ya elfu kumi ambao walijitosa kwenye kinyanganyiro cha kutafuta tiketi za chama cha CCM mwezi Agosti mwaka huu, ili kutafuta viti vya ubunge kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania.

Baada ya kupata tiketi hiyo Hamis Mwinjuma aliingilia Kampeni, uchaguzi ukafanyika Jumatano 28 Oktoba mwaka huu na akamshinda Yosepher Komba wa CHADEMA.

Mwana Fa alizoa kura 47,578 huku Komba akipata kura 12,034. Sio mengi yanafahamika kuhusu familia ya Mwana Fa ila alifunga ndoa mwana 2016 na binti kwa jina Helga na arusi ilihudhuriwa na watu wachache tu licha ya kwamba yeye ni mtu maarufu.

Mwanamuziki huyo aliingilia fani hiyo mwaka 1995 akiwa bado anasoma shule ya upili na hadi sasa ameendelea kufurahia uungwaji mkono wa mashabiki wake na wapenzi wa muziki nchini Tanzania.

Mhusika mwingine wa sanaa nchini Tanzania ambaye ameingia bungeni kupitia uchaguzi mkuu wa hivi punde ni meneja wa wasanii maarufu kama Babu Tale ambaye ni mmoja wa walioanzisha WCB.

Meneja huyo ambaye jina lake halisi ni Hamisi Shabaan Tale Tale wa chama cha CCM hakuwa na mpinzani katika kuwania kiti cha ubunge eneo la Morogoro Kusini Mashariki na hilo lilisababisha atangazwe mshindi.

Mwaka huu umekuwa wa huzuni na furaha kwake kwani alifiwa na mke wake kwa jina Shammy mwisho wa mwezi juni na sasa amepiga hatua maishani na kuwa kiongozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *