Mwalimu akatazwa kufunza chekechea kwa sababu ya “tattoo”

Mwalimu mmoja wa shule ya msingi nchini Ufaransa au ukipenda France maajuzi alikatazwa asifunze watoto wadogo au ukipenda watoto wa chekechea kisa na maana michoro kwenye ngozi yake yaani “tattoo”.

Mwalimu huyo wa kiume kwa jina Sylvain Helaine wa umri wa miaka 35 amefunika mwili wake mzima na tattoo na hata kubadili rangi ya macho yake kuwa nyeusi tititi!

Mambo yalichacha pale mzazi mmoja alipokwenda shuleni katika shuleni kulalamika kwamba mwanawe alipatwa na ndoto mbaya baada ya kumwona mwalimu Helaine.

Ndiposa usimamizi wa shule ukaamua kwamba asiwafunze watoto wa umri mdogo ila anaruhusiwa kufunza walio na miaka sita na zaidi.

Sylvain amekuwa mwalimu katika shule ya “Docteur Morere Elementary School” kwa muda na katika kujieleza alisema alitaka wanafunzi wake wazoee kwamba siku za usoni watakutana na binadamu wa kila aina na rangi.

Ulimi wake pia umetiwa rangi nyeusi na kufikia sasa anasemekana kuwa raia wa france mwenye tatoo nyingi zaidi.

Mwalimu Sylvain Helaine

Nchini Kenya hakuna sheria ya kudhibiti michoro ya ngozi ila watu wana maoni tofauti. Mwanzo wa mwaka huu wanafunzi wapatao kumi walifukuzwa na usimamizi wa shule ya upili ya Mtakatifu Maria huko Nyeri baada ya kupatikana na michoro hiyo ya ngozi.

Mmoja wa wanafunzi hao alisema anapenda sanaa na tattoo ni aina ya sanaa na alipokwenda kuchorwa, mchoraji hakuwa na swali lolote kuhusu umri au kibali.

Waajiri wengine nchini Kenya pia hawakubali michoro kama hiyo kama vile uanajeshi, huwezi kujiunga na vikosi hivyo iwapo una tattoo.

Wakenya wengi pia ni wakristo ambao hutumia Biblia kama kigezo cha maadili na imezungumza kinyume na michoro hiyo. Kifungu cha 19 mstari wa 28 katika kitabu cha “Mambo ya Walawi”, kinasema ‘Msichanje chale yoyote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana.’

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *