Categories
Michezo

Mvutano kati ya FKF na timu 4 watishia kuathiri msimu mpya wa ligi kuu

Shirikisho la kandanda nchini Fkf litaziadhibu  timu ambazo hazitasaini mkataba wa  kupeperusha mechi za ligi kuu inayotazamiwa kuanza Jumamosi hii.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi  mapema Alhamisi ,mwenyekiti wa Fkf Nick Mwendwa amesuta vilabu vinne ambavyo havijasaini mkataba huo wa matangazo ya runinga akisisitiza kuwa vimepewa nafasi ya mwisho kubatilisha misimamo yao mikali na kuruhusu ligi kuanza bila tashwishwi.

Rais wa FKF Nick Mwendwa akizungumza wakati wa kuzindua mkataba baina ya FKF na Star Times

“Sisi tuko tayari kuanza ligi Jumamosi bila hizo timu nne ambazo hazijasaini mkataba huo,lakini pia tunawapa nafasi ya kufikiria upya kuhusu uamuzi wao ,la sivyo tutachukua hatua kama shirikisho wiki ijayo,hakuna vile timu hizo zitazuia ligi kuanza”akasema Mwendwa

Mwendwa amekariri kuwa haki zote za ligi ya Kenya zinamilikiwa shirikisho na wala sio za vilabu inavyodaiwa .

“Fkf ndio wameliki wa haki zote za soka humu nchini na pia ligi ya Fkf Premier League,kwa hivyo tusidanganyane ,si bado tunaomba timu za Zoo Fc,Gor Mahia ,Mathare United na Ulinzi Stars kutafakari na kubadilisha msimamo wao ligi ianze vijana wapate doo”akaongeza Mwendwa

Nick mwendwa akiwa na CEO wa Star Times  Hanson Wang katika uzinduzi wa mkataba ligi kuu FKF

Fkf imezindua mkataba wa miaka 7 na kampuni ya Star Times ya kutoka China ili kupeperusha mechi za ligi kuu ambapo inatarajiwa kuwa angaa mechi 100 zitarushwa kwenye runinga kila msimu .

Hata hivyo kwenye mahojiano na Kbc kwa njia ya simu mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier ameapa kuelekea mahakamani kusimamisha mkataba huo wa runinga na kupinga hatua ya Fkf Kumiliki haki zote za vilabu.

“Mimi kwa sasa sina wakati wa kujibizana na Fkf lakini nitafuata mkondo wa sheria ambapo nitaelekea mahakamani kutaka kusimamishwa kwa mkataba huo kwa sababu haki za vilabu hazipaswi kutwaliwa na shirikisho”akasema Rachier

Utata huo huenda ukaibuka mvutano mkubwa kwenye ligi kuu ambayo iliratibiwa kuanza Jumamosi hii ambapo jumla ya mechi 3 zimeratibiwa kupeperushwa kupitia Runinga ya Star Times.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *