Muziki wangu sio wa watoto!!! Cardi B

Mwanamuziki Cardi B amesema kwamba muziki ambao yeye hufanya haulengi watoto wadogo bali ni wa watu wazima. Hii ni baada ya kuingiliwa na mashabiki kwenye mitandao kulingana na hatua aliyoichukua mnamo mkesha wa mwaka mpya.

Siku hiyo ya mwisho ya mwaka 2020, Cardi B alikuwa mubashara kwenye akaunti yake ya Instagram, akiimba na kuuchezea wimbo wake kwa jina ‘WAP’ ambao amemshirikisha mwanamuziki Megan Thee Stallion.

Cardi B anazima wimbo huo mara moja baada ya binti yake wa miaka miwili Kulture kuingia chumbani alikokuwa. Video hiyo ilisambazwa sana kwenye mitandao ya kijamii huku wengi wakitaka kujua ni kwa nini aliuzima wimbo huo.

Mwanamuziki huyo kupitia Twitter alisihi mashabiki wake waache kumwingilia akisema yeye sio ‘Jojo Siwa’. (Jojo Siwa ni mcheza densi wa Marekani ambaye sasa ana umri wa miaka 17).

Anaendelea kusema, “Muziki ninaounda sio wa watoto bali ni wa watu wazima, kila mzazi ana jukumu la kusimamia anachosikiliza mwanawe. Mimi huzungumzia na kuimba kuhusu ngono lakini sio kwa mwanangu na kila mzazi anafaa kufanya hivyo.”

Anajitetea akisema kuna kina mama ambao hucheza densi uchi usiku kucha katika sehemu za burudani kama njia ya kujipatia mapato na hawafanyi hilo wakiwa karibu na wanao. “Acheni kuzua mjadala kuhusiana na jambo hili. Ni jambo la mtu kutumia akili.” aliandika Cardi B kwenye Twitter.

Mwanadada huyo ambaye ni mke wa mwanamuziki Offset anasema namna anachagua kulea mtoto wake haifai kukwaza mtu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *