Categories
Habari

Muungano wa Watumishi wa Umma wamtaka Rais Kenyatta atatue mgomo wa wahudumu wa afya

Muungano wa Watumishi wa Umma nchini sasa unamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati kwenye mgomo unaoendelea wa wahudumu wa afya ili kupata suluhu la kudumu.

Maafisa wa muungano huo waliozungumzia athari mbaya kwa vituo vya afya ya umma pia wametoa wito kwa pande husika kulegeza misimamo kwa ajili ya Wakenya wanaoteseka.

Wakiongozwa na Naibu Katibu, Jerry Ole Kina, maafisa hao wametoa wito wa mashauriano baina ya pande husika, wakikariri kwamba msimamo huo mkali unawaathiri Wakenya maskini.

Muungano huo umemkosoa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwa kutishia kuwafuta kazi wahudumu wa afya wanaogoma, ukisema iwapo hatua hiyo itatekelezwa itaathiri vibaya sekta ya afya ambayo tayari inakumbwa na changamoto.

Ole Kina amesema changamoto zinazowakumba wahudumu wa afya zilitokana na ugatuzi na suluhisho linaweza kupatikana kwa njia ya mashauriano kati ya serikali kuu na zile za magatuzi.

Wauguzi na matabibu waligoma mnamo tarehe saba mwezi huu wakishinikiza, miongoni mwa maswala mengine, marupurupu ya mazingira hatari ya kazi na hali bora za kazi huku wakiongoza katika vita dhidi ya janga la COVID-19.

Madaktari pia walijiunga kwenye mgomo huo Jumatatu wiki hii wakitoa shinikizo sawa na hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *